Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imeelezea wasiwasi kuhusu adhabu iliyotolewa leo na mahakama ya China ya kifungo cha miaka minne jela dhidi ya mwanahabari wa Kichina Zhang Zhan ambaye aliangazia mlipuko wa kwanza wa virusi vya corona katika mji wa Wuhan.
Zhan ambaye ni wakili wa zamani, amehukumiwa katika mahakama ya Shanghai kwa madai ya "kuchochea ugomvi" wakati akiripoti matukio ya mwanzo ya mripuko wa corona.
Ofisi hiyo imesisitiza mwito wake wa kutaka Mwanahabari huyo aachiliwe huru.
Ripoti zake za moja kwa moja na makala zilisambazwa kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii Februari, na kuwafikia maafisa nchini humo ambao mpaka sasa wamewaadhibu watu nane waliofichua habari za kirusi hicho.
Umoja wa Mataifa umesema uliilalamikia serikali ya China katika mwaka huu wote wa 2020 ukisema kesi hiyo ni mfano kwa ukandamizaji wa kupindukia dhidi ya uhuru wa kujieleza unaohusiana na COVID-19.