Star Tv

Siku moja baada ya sehemu ya soko maarufu la bidhaa na urembo maarufu kama makoroboi jijini Mwanza kuteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa,wafanyabiashara katika eneo hilo wamelipongeza jeshi la zimamoto kwa juhudi zilizosaidia kudhibiti moto huo na kuokoa sehemu kubwa ya soko hilo.

Taarifa na Leonard Mapuli

Waswahili husema mtafutaji hachoki na akichoka basi kapata…..usemi huu wa wahenga huenda ni faraja tosha inayowafariji wathirika waliopoteza mali zao kwa moto usiku wa kuamkia jumatano.

Shughuli za kuvijenga upya vibanda vilivyoteketea kwa moto ndio jambo linashuhudiwa ndani ya soko hilo huku wafanyabiashara ambao mali zao hazikuteketezwa na moto wakiendelea na biashara zao.

Licha ya janga hilo la moto kuacha makovu na vidonda kwa wengi limetonesha kidonda cha Kulwa Makasi ambaye ni manusura wa kifo kufuatia kupigwa risasi mbili miguuni na polisi miaka 9 iliyopita katika eneo hilo la soko la Makoroboi wakati wa vurugu za mgambo kuwaondoa machinga katika eneo hilo la Makoroboi.

Mpaka sasa Kulwa anaishi na risasi mbili mwilini mwake ambazo zinahitaji fedha ili zitolewe, wakati huohuo akidunduliza pesa kwa lengo la kuyawezesha maisha yake yaende akiwa na kibanda kimoja kati ya vibanda 65 vilivyoteketea kwa moto usiku wa  kuamkia jumatano.

Uchangamfu kwa wafanyabiashara wengi katika eneo hilo ni kama umekwenda likizo kutokana na janga hilo la moto , zaidi ni tathmini na majuto ya wapi watapata pesa ya kusimama tena kibiashara.

Ernest Matondo ambaye ni mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wadogo Tanzania, licha ya kibanda chake kuteketea anasema kazi iliyofanywa na jeshi la zimamoto haikuwa haba kwani imesaidi kuokoa mali za watu wengine.

Ambwene Mwakibwete ambaye ni Kamanda wa kikosi cha zimamoto Mwanza amesema uzimaji wa moto si kipaumbele kikubwa kwa jeshi hilo bali kuzuia kabisa moto na majanga mengine na amewasihi wananchi kujitokeza mara zote katika maonesho ya jeshi hilo ili kuzuia majanga mbalimbali ikiwemo moto.

Jumla ya matukio 113 ya majanga ya moto yaliripotiwa mwaka 2019 mkoani Mwanza huku majanga 29 yakifanikiwa kupata uokozi toka kwa jeshi la zimamoto.

Tukio la moto kwenye soko la makoroboi linakuwa la 17 tangu kuanza, na kwa mwaka 2020 likiwa tukio la 3 kufanikiwa kupata uokozi wa jeshi hilo huku jumla ya wafanyabiashara 159 wakipata hasara ya kuunguliwa na vibanda vyao.

Mwisho.

Latest News

SHAMBULIO LA KOURÉ NCHINI NIGER LAMUUMIZA KICHWA MACRON.
11 Aug 2020 16:07 - Grace Melleor

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameitisha kikao na baraza la ulinzi nchini mwake kufuatia Shambulio la Koure nchini Nig [ ... ]

NEEMA YAWASHUKIA WAKULIMA NCHINI.
11 Aug 2020 15:57 - Grace Melleor

Katika kuhakikisha kwamba tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo inaongezeka ili kujitosheleza kwa chakula na malighafi z [ ... ]

CHANJO YA COVID-19 YAIDHINISHWA KWA MATUMIZI URUSI.
11 Aug 2020 13:34 - Grace Melleor

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kwamba chanjo iliyotengenezwa ndani ya Urusi kwa ajili ya ugonjwa wa Covid-19 imeid [ ... ]

Other Articles

Social Media

Copyright © 2020 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.