Star Tv

Kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Boko Haram nchini Nigeria Abubakar Shekau, amejiua mwenyewe, wanamgambo wa kundi hasimu wamesema katika sauti iliyorekodiwa.

Katika rekodi ya sauti iliyopatikana na mashirika ya habari, kundi la Islamic State katika mkoa wa Afrika Magharibi (Iswap) lilisema Shekau alifariki baada ya kujilipua kwa kutumia vilipuzi wakati wa mapigano kati ya makundi hayo mawili.

Shekau aliripotiwa kufariki mwezi uliopita na awali ashawahi kuripotiwa kuuawa lakini baadaye alionekana akiwa hai.

Kundi la Boko Haram na serikali ya Nigeria bado havijathibitisha kifo chake.

Katika sauti ambayo haikuwa na tarehe iliyorekodiwa, sauti inayodhaniwa kuwa ya kiongozi wa Iswap Abu Musab al-Barnawi ilisema Shekau "alijiua kwa kujilipua na vilipuzi".

Wapiganaji wa Iswap walimsaka mbabe huyo wa kivita na kumpatia nafasi ya kutubu na kujiunga nao, al-Barnawi alisema.

Msemaji wa jeshi Brigedia Jenerali Mohammed Yerima aliiambia BBC wakati huo kwamba jeshi lilikuwa linachunguza kile kilichotokea, lakini halitatoa taarifa hadi lipate uthibitisho rasmi.

Mwandishi mmoja aliye na uhusiano wa karibu na vyombo vya usalama alisema kuwa Shekau alikufa wakati Iswap iliposhambulia ngome za Boko Haram katika msitu wa Sambisa, kaskazini mashariki mwa Nigeria

Baada ya kuchukua uongozi wa of Boko Haram mwanzilishi wake alipofariki katika kizuizi cha polisi mwaka 2009, Shekau aliongoza mabadiliko yake kutoka kwa dhehebu la kawaida hadi uasi mbaya ambao umeenea kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

Chini ya uongozi wa Shekau, Boko Haram walifanya mashambulio ya mabomu, utekaji nyara na kuvamia magereza katika eneo hilo.

Kuanzia mwaka 2014, kundi hilo lilianza kuvamia miji katika juhudi za kuunda jimbo la Kiislamu kwa kutumia sheria za Kiislamu.

Akisadikiwa kuwa na miaka arobaini na kitu, Shekau aliunga mkono kampeni ya umwagaji damu katika video za propaganda ambazo zililinganishwa na Osama Bin Laden.

"Nafurahia kuua ... jinsi ninavyofurahia kuchinja kuku na kondoo," - Alisema Shekau katika moja ya video hizo mwaka 2012.


Kundi hilo pia lilipata umaarufu kimataifa mwaka 2014 wakati lilipowateka nyara mamia ya wasichana katika shule moja mjini Chibok katika jimbo la Borno na kuchochea harakati za #BringBackOurGirls, Ambapo mpaka sasa wengi wao hawajulikani waliko.

Muda mfupi baadaye, Marekani ilimtaja Shekau kuwa gaidi wa kimataifa na kutangaza zawadi ya dola milioni saba kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwake.
#ChanzoBBCSwahili

Latest News

NIGERIA YAPOKEA NDEGE SITA ZA KUPAMBANA NA WAASI.
23 Jul 2021 14:50 - Grace Melleor

Nigeria imepokea ndege sita za kijeshi iliyonunua kutoka Marekani, ambazo zinatarajiwa kupiga jeki juhudi za kukabiliana [ ... ]

WATU KADHAA WAKAMATWA KWA JARIBIO LA KUTAKA KUMUUA RAIS RAJOELINA.
22 Jul 2021 13:15 - Grace Melleor

Raia kadhaa wa mataifa ya kigeni pamoja na wengine wa nchini Madagascar wanashikiliwa na mamlaka nchini humo kwa tuhuma  [ ... ]

HABARI ZA HIVI PUNDE: ANNA MGHWIRA AFARIKI DUNIA.
22 Jul 2021 10:55 - Grace Melleor

Aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amefariki dunia leo Julai 22, katika Hospitali ya Mount Meru.

Other Articles

Social Media

Copyright © 2021 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.