Star Tv

Kiongozi wa Harakati la Sadr nchini Iraq ametoa wito kwa wananchi  kufanya maandamano ya watu wasiopungua milioni moja ya kulaani kuwepo kijeshi Marekani nchini humo.

Muqtada Sadr ambaye ni kiongozi wa kundi hilo la harakati ametoa wito huo siku kadhaa baada bunge la Iraq kupitisha mpango wa kuwatimua askari vamizi wa jeshi la Marekani ambalo kwa mujibu wao wanalitambua kama jeshi la kigaidi katika ardhi ya nchi hiyo.

Kiongozi huyo wa Harakati za kundi la  Sadr amesema kupitia ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter ameandika  kwamba, "anga, ardhi na mamlaka ya kujitawala ya Iraq yanakiukwa kila siku na majeshi vamizi ikiwemo Marekani". 

Aidha, siku ya maandamano bado haijatangazwa mpaka sasa, na kiongozi Sadr amewataka wananchi wa Iraq wafanye maandamano ya amani na ya umoja, kwa  idadi hiyo ya watu milioni moja kulaani uwepo wa jeshi la  Marekani ndani ya nchi ya Iraq  na  akisema  uwepo wa jeshi hilo ni ukiukwaji unaofanya nchini humo.

Kufuatia kuuliwa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Abu Mahdi Al Muhandis, naibu Mkuu wa Al-Hashdu-Sha'abi wa Iraq katika shambulio la kigaidi lililofanywa na Marekani ndani ya ardhi ya Iraq, mnamo tarehe 5 Januari bunge la nchi hiyo lilipitisha mpango wa kuitaka serikali iyatimue majeshi ya kigeni na kufuta ombi lake la kupatiwa msaada na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani kwa ajili ya kupambana na kundi la kigaidi  la ISIS.

Kiongozi Muqtada Sadr alikosoa vikali mpango huo uliopitishwa na bunge, akisema ni "Jibu dhaifu" sambamba na kutaka kufutwa mara moja makubaliano ya usalama yaliyosainiwa kati ya Iraq na Marekani na pia kufunga ubalozi wa Marekani ulioko nchini humo, kufukuza  askari wa nchi hiyo na kutambulika kuwa ni kosa la jinai kuanzisha mawasiliano na serikali ya Washington.

                                                                                                  Mwisho.

Copyright © 2020 . Star Tv - Tanzania. All Rights Reserved.